Hivi Ndivyo Edward Lowassa Anavyoishi Kama Rais nje ya Ikulu...
Edward Lowassa |
Kwa mujibu wa matangazo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Lowassa aliyekuwa akichuana kwa karibu na Magufuli katika muda wote wa kampeni za miezi miwili zilizoanza Agosti 21, 2015, alishika nafasi ya pili baada ya kupata asilimia 39.97 ya kura zote halali zilizopigwa.
Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata asilimia 58.46 ya kura hizo na aliapishwa Novemba 5, 2015 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tangu wakati huo ameendelea kusimamia mabadiliko kadhaa katika serikali yake ya awamu ya tano.
Hata hivyo, Nipashe imebaini kuwa licha ya Lowassa kutotangazwa mshindi na kuingia Ikulu, mgombea huyo wa urais wa mwaka jana amekuwa na mwenendo wa matukio yanayofanana kwa kiasi kikubwa na ya kiongozi dola.
Lowassa alipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu akidai alipokwa ushindi na NEC kwavile takwimu zake zinaonyesha alipata asilimia 60 ya kura zote halali.
Katika uchunguzi wake huo uliohusisha baadhi tu ya matukio, Nipasahe imebaini kuwa Lowassa ameendelea kufanya hafla na matukio makubwa kama Rais licha ya kuwa kwake nje ya Ikulu.
“Bungeni kuna mawaziri kivuli… na sasa Lowassa ni kama Rais Kivuli kwa sababu baadhi ya matukio huhusika akiwa kama kiongozi mmoja mkubwa katika nchi,“ mmjoja wa wachambuzi aliiambia Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina.
Kadhalika, katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa baadhi ya matukio yanayomfanya Lowassa aishi kama rais nje ya ikulu ni kukutana kwake na wafanyabiashara, kualikwa kama mgeni rasmi na kukutana na Balozi wa Japan.
Pia amewafunda mameya na wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wanachi (Ukawa), mwamvuli wa kisiasa ambao Chadema ni mwanachama wake, kwa kuwapa onyo kuwa wasipotimiza ndoto za wananchi watachukuliwa hatua. Mambo hayo, yamefanywa pia kwa nyakati tofauti na Rais John Magufuli.
ATETA NA MAALIM SEIF
Novemba 13, mwaka jana Lowassa alikutana na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad na kujadiliana naye juu ya mkwamo wa kisiasa wa Zanzibar miongoni mwa masuala mbalimbali.
Lowassa alifanya hivyo baada ya Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kumtembelea kwenye ofisi zake binafsi zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Kadhalika, Januari 24 Lowassa alikutana na Maalim Seif kwa mara nyingine tena mjini Dodoma na kujadili masuala ya Zanzibar, kabla wote kwa pamoja hawajakutana na wabunge wa Ukawa kutoka Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Rais Magufuli aliwahi pia kukutana na Maalim Seif, Ikulu jijini Dar es Salaam na kujadiliana naye masuala kadhaa kuhusiana na hatma ya Zanzibar baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo. Kikao hicho cha Rais Magufuli na Malim Seif kilifanyika Desemba 21, mwaka jana.
AMTEMBELEA SUMAYE MUHIMBILI
Januari 11 , Rais Magufuli alifanya ziara ya kwenda kumjulia hali Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Siku mbili baadaye, yaani Januari 13, Lowassa alifanya hivyo pia, akienda kumtembelea Sumaye ambaye walikuwa naye bega kwa bega katika uchaguzi mkuu uliopita baada ya kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutua Chadema kama alivyofanya Lowassa.
APOKEWA KWA KISHINDO NA WAKAZI DAKAWA
Januari 24 Lowassa aliyekuwa njiani kuelekea Dodoma, alikutana kwa muda na wananchi waliomsimamisha barabarani katika eneo la Dakawa mkoani Morogoro.
Lowassa alizungumza kwa muda na wananchi hao na kushangiliwa kwa nguvu kabla ya kuendelea na safari yake.
Lowassa alifanya hivyo ikiwa ni siku mbili tu zimepita (Januari 21, 2016) tangu Rais Magufuli apokewe pia kwa kishindo na wakazi wa Arusha wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.
Mamia ya wananchi walijitokeza kumsikiliza Rais Magufuli aliyekuwa amevalia magwanda ya kijeshi.
AFUNDA MAMEYA UKAWA DAR
Januari 18, Lowassa alikutana na mameya wanaotoka Ukawa wa Manispaa za Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuzungumza nao masuala kadhaa kabla ya kuwaonya kuwa watatimuliwa iwapo hawatatimiza lengo la kuwatumikia wananchi kwa namna inayotarajiwa, ikiwamo kuinua mapato, kuboresha usafi, kukomesha ubadhirifu kwenye manispaa zao na pia kushughulikia kero ya foleni jijini humo.
Tukio linalofanana na hilo limefanywa mara kadhaa na Rais Magufuli, ikiwamo Novemba 7, mwaka jana wakati alipokutana na makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu ambao aliwapa maelekezo ya kazi huku akiwaonya kuwa atakayeshindwa kwenda na kasi katika kushughulikia kero za wananchi hataachwa.
AKUTANA NA BALOZI WA JAPAN
Januari 18, Lowassa alikutana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida wakati wa kusaini mikataba ya miradi mitatu yenye thamani ya Dola 204,300 kwa ajili kusaidia Shule ya Kingolwira, Morogoro, Shule ya Muyuni na Kituo cha Afya cha Lutheran kilichopo Arusha.
Rais Magufuli, kwa nafasi yake, ameshakutana pia na mabalozi kadhaa ikiwamo Novemba 30, mwaka jana wakati alipokutana na mabalozi wa China na Korea.
AKUTANA NA WAFANYABIASHARA
Januari 14, Lowassa alitembelewa ofisini kwake, Mikocheni na wafanyabiashara kadhaa wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuzungumzia nao masuala mbalimbali.
Tukio kama hilo limewahi pia kufanywa na Rais Magufuli Desemba 3, mwaka jana wakati wa mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara, alipokutana Ikulu na wafanyabiashara wakubwa na kubadilishana nao mawazo.
WASEMAVYO ZAIDI WACHAMBUZI SIASA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, akizungumza na Nipashe, alisema Lowassa ni mwanasiasa mahiri, aliyebobea na anayejua anachokifanya.
Alisema anajitajidi asisahaulike kwenye ramani ya siasa na nyoyo za Watanzania.
"Kwa sasa hana nafasi ndani ya Chadema zaidi ya kutambulika aliyekuwa mgombea urais ambayo siyo nafasi rasmi ilishaisha wakati wauchaguzi mkuu, haendi bungeni, haudhurii vikao vya madiwani labda aalikwe Monduli, atajulikanaje anachofanya ndiyo maana atafuta fursa na nafasi ili aendelee kuwepo ndani ya mioyo ya watanzania," alisema.
Aidha, aliishauri Chadema kuangalia namna ya kumpa wadhifa ndani ya chama hicho ili awe na shughuli za kila siku za kichama na kwamba kama ana nia ya kuimarisha upinzani nchini kwa kutumia nafasi hiyo, atafanya mambo mengi.
Alisema baada ya chama hicho kumpoteza aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Willbriad Slaa, sasa wanahitaji mtu mwenye mbinu na mikakati kama Lowassa awepo ndani ya uongozi na kufanya shughuli za kila siku.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema Lowassa ni mwanasiasa wa upinzani na hivyo ana hiari ya kuendelea na shughuli za siasa za kuimarisha chama chake na nyinginezo, hivyo haoni kama kuna tatizo juu ya kile anachokifanya hasa kwa kutambua vilevile kuwa ni waziri mkuu mstaafu.
“Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Lowassa amekuwa kimya hajafanya chochote kikubwa ukilinganisha na wanasiasa wa nchi jirani kama Kenya (Raila Odinga).
Amekuwa akifanya mikutano ya hadhara na shughuli nyinginezo," alibainisha na kuongeza:
"Anachofanya Lowassa ni siasa za kawaida. Lazima akutane na wapiga kura na makundi mbalimbali ikiwa kuiwashukuru wapigakura.”
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema anachofanya Lowassa ni kwa sababu anatambua nafasi yake katika jamii kuwa ana wafuasi wake na wa Ukawa ambao wanamhitaji hivyo ni lazima akutane nao.
“Ni mapema sana kwa sababu mwezi Oktoba mwaka jana, uchaguzi umemalizika hadi sasa tupo kwenye kipindi cha mpito. Kulikuwa na nia ya Ukawa kushukuru wapigakura lakini wamewekewa vikwazo… siyo Rais kivuli,” alisema Baregu.
“Kila mtu ana haki ya kukutana na yeyote au kundi lolote alimradi hajavunja sheria wala kwenda kinyume cha Katiba.”
0 comments: