News:Siri ya Kuahirisha Uchaguzi wa Meya Dar Yajulikana..Ukawa Wadai CCM Ikimwaga Ugali wao Wanamwaga Mboga
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwamvuli wa Ukawa kimetaja mambo matatu ambayo ndiyo yamechangia kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliokuwa umepangwa kufanyika leo.
Taarifa ya Halmashauri ya Jiji iliyotolewa jana haikueleza sababu za kuahirisha uchaguzi huo zaidi ya kusema kuwa utafanyika katika siku itakayotangazwa baadaye.
Msemaji wa jiji, Gatson Makwembe hakutaka kuzungumzia sababu za kuahirisha uchaguzi huo.
“Siwezi kuzungumza mengi kwa sasa, ila ninachoomba wakazi wa Dar es Salaam wavute subira hadi tutakapotangaza siku ya kufanyika uchaguzi huu,” alisema Makwembe.
Juzi, Makwembe aliliambia gazeti hili kuwa walishapewa maelekezo kutoka ngazi za juu yaliyowataka kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika Januari 23. Kwa mujibu wa katibu wa Chadema wa Kanda, Henry Kilewo, mambo hayo ni CCM kutaka kujipanga kuwarejesha wajumbe wake waliotimuliwa kwenye uchaguzi wa meya wa Ilala na Kinondoni, kuhofia upinzani kushinda kutokana na idadi yao, na hofu kuwa meya kutoka upinzani atafichua uozo unaotokana na jiji kuwa chini ya utawala wa CCM kwa muda mrefu.
“Mambo hayo matatu ndiyo ambayo yanawapa hofu CCM na kutumia nafasi yake ya chama tawala kuagiza jiji kuahirisha uchaguzi,” alisema Kilewo.
“Wakithubutu kuwaingiza wajumbe hao, na sisi tutafanya hivyohivyo. Waache wamwage ugali Ukawa tutamwaga mboga.”
Madiwani 161 kutoka halmashauri hizo wanatarajiwa kupiga kura kumchagua meya mpya atakayemrithi Didas Masaburi, ambaye alihamishia harakati zake za kisiasa kwenye ubunge wa Ubungo, lakini hakufanikiwa.
Kati ya madiwani hao, 87 wanatoka Ukawa, wakati 74 wanatoka CCM. Kwa maana hiyo CCM imezidiwa wajumbe 13 na vyama vya Chadema na CUF ambavyo vimeshinda viti vingi vya udiwani wilayani Ilala na Kinondoni.
Kilewo alisema wajumbe wa CCM ni wachache ukilingalisha na Ukawa, hivyo wamelazimika kufanya hivyo wakisubiri wajumbe ambao ni mawaziri wamalize vikao vya Bunge ndipo wahudhurie.
Kilewo alikitaka chama hicho tawala kujiandaa kisaikolojia kwani kuna maisha baada ya uongozi.
“Wanajua muziki wa Ukawa tukilishika jiji hili, tutakwenda kufumua uozo wao wote walikuwa wameuficha na kuwakosesha ulaji baadhi ya viongozi wao,” alisema Kilewo.
Kwa upande wake, Katibu Uenezi wa CCM mkoani Dar es Salaam, Juma Simba ‘Gadaffi’ alisema CCM haihusiki na kuingiza wajumbe katika baraza la madiwani, bali Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ndiyo yenye mamlaka hayo.
“Tatizo lao hawa wapinzani kila kitu wanapinga, hata wajumbe walioteuliwa na Rais kisheria hawataki washiriki katika baraza, halafu ndiyo wanasema wanafuata sheria?” alihoji Gadaffi.
Alisema CCM ni chama makini na kinafanya maamuzi ya busara, kwa kuwa kimemteua mgombea wa umeya aanayekubalika na kila mtu, tofauti na mshindani wake.“Usishangae hata huu uchaguzi wa meya wa jiji wajumbe wa upinzani wakatupigia kura kama walivyofanya kule Temeke, kwa sababu ya umakini wa CCM ya kuweka mtu anayekubalika,” alisema Gadaffi.
0 comments: