CUF Kuandamana Kupinga Marudio Ya Uchaguzi Zanzibar
CHAMA
cha Wananchi (CUF) Bukoba kimejiandaa kufanya maandamano ya amani
keshokutwa, kwa ajili ya kupinga kufanyika upya uchaguzi wa Zanzibar
unaotarajiwa kuwa Machi mwaka huu.
Kimeiomba
pia serikali ya awamu ya tano, kuchukua uamuzi wa kumtambua Maalim Seif
Sharif Hamad kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais Zanzibar na kuwa
hakiko tayari kurudia uchaguzi huo tena.
Akizungumza
na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho, Kaimu Mwenyekiti
wa chama hicho Saverina Mwijage, alisisitiza kuwa kamwe chama hicho
hakitakuwa tayari kurudia uchaguzi huo uliotangazwa na Tume ya uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC) kuwa utafanyika Machi 20,kwa kile kinachodaiwa ni
kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25,mwaka jana.
“Tumedhamiria
kuandamana ili kumfikishia ujumbe wetu Rais John Magufuli kupitia kwa
Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella lengo letu hasa ni kupinga
uchaguzi wa Zanzibar. Hali ya Zanzibar kwa sasa haiko shwari, watu
wanatishiwa maisha yao, wanaishi kwa hofu juu ya maisha,” alisisitiza.
Mwijage
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Taifa,
alisema chama hicho kinatambua uchaguzi ulishakwisha na tume hiyo
ilishatoa vyeti kwa walioshinda, kwa mantiki hiyo CUF inamtambua Maalim
Seif kuwa alishinda katika uchaguzi huo.
Alisema
maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00
alasiri na baadaye utakuwepo mkutano wa hadhara katika Uwanja wa
Mashujaa Mayunga ulioko mjini Bukoba ili kuutangazia umma juu ya msimamo
wa chama hicho na baada ya hapo watazunguka katika wilaya za Muleba,
Missenyi na Karagwe.
0 comments: