TCU Yafuta Vyuo Vishiriki Vya Mtakatifu Joseph.....Wanafunzi Watakiwa Kuondoka Chuoni Mara Moja, Watapangiwa Vyuo Vingine
KUFUTWA KWA
KIBALI KILICHOANZISHA VYUO VIKUU VISHIRIKI VYA SAYANSI ZA
KILIMO NA TEKNOLOJIA (SJUCAST) NA TEKNOLOJIA YA HABARI
(SJUCIT) VYA CHUO KIKUU CHA MT. YOSEFU TANZANIA (SJUIT), KAMPASI YA SONGEA
1. Tunapenda kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt.
Yosefu Tanzania (SJUIT) ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Chuo hiki kinamilikiwa na Shirika la Kitawa la Dada
wa Maria Imakulata (DMI) pamoja na washirika wao. Hapa nchini chuo hiki
kilianzishwa mwaka 2003 chini ya usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
(NACTE). Mnamo mwaka 2011, chuo hiki kiliwasilisha maombi ya kusajiliwa na TCU.
Maombi hayo yaliidhinishwa na Tume tarehe 14 Desemba, 2011. Kisha tarehe 27
Septemba, 2012 kufuatia maombi ya uongozi wa Chuo, Tume iliidhinisha kuanzishwa
kwa Vyuo Vikuu Vishiriki vitatu ambavyo ni: Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za
Kilimo na Teknolojia (St. Joseph
University College of Agricultural Science and Technology - SJUCAST), na
Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari (St. Joseph University College of Information Technology - SJUCIT)
ambavyo vilianzishwa Songea; na Chuo Kikuu Kishiriki cha Uongozi, Uhasibu na
Fedha (St. Joseph College of Management,
Accounting and Finance - SJUCMAF) kilichopo Makambako, Njombe. Hivi sasa
Chuo Kikuu hiki kina Kampasi nyingine Arusha, Boko na Luguruni, Dar es Salaam,
huku Makao Makuu yakiwa katika Kampasi ya Luguruni.
2. Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo
Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na
kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.
3. Kwa muda mrefu katika Vyuo Vikuu Vishiriki vya Sayansi
za Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Teknolojia ya Habari (SJUCIT) kumekuwapo
na mlolongo wa matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za
uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu.
Jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu kukitaka Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania
(SJUIT) kuhakikisha hivi Vyuo Vikuu Vishiriki vinatoa elimu inayokidhi viwango
vya ubora vilivyowekwa na Tume hazikupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo.
Matokeo yake wanafunzi wa SJUCAST na SJUCIT wamekuwa hawapati elimu kwa kiwango
stahiki. Hivi sasa katika vyuo hivi vishiriki viwili kuna jumla ya wanafunzi
2046 wanaosoma programu za digrii zifuatazo:
a)Bachelor of
Technology in Agriculture [B. Tech. in Agriculture] (wanafunzi 282)
b)Bachelor of
Technology in Horticulture [B. Tech. in Horticulture] (wanafunzi 61)
c)Bachelor of
Technology in Agricultural Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.]
(wanafunzi 255)
d)Bachelor of
Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.]
(wanafunzi 238)
e)Bachelor of
Science with Education (wanafunzi 732)
f)Bachelor of
Science in Computer Science (wanafunzi 250)
g)Bachelor of
Computer Science with Education and Bachelor of Science in
Education
with Computer Science (wanafunzi 196)
h)Diploma in
Computer Science (wanafunzi 81)
4.Kutokana na yaliyobainishwa hapo awali, tunapenda
kuuarifu umma kwamba, Tume imejiridhisha kuwa hivi Vyuo Vikuu Vishiriki viwili
havitoi elimu ya chuo kikuu ya viwango stahiki. Kwa kuzingatia ukweli kwamba
wanafunzi katika vyuo hivi vishiriki vya SJUCAST na SJUCIT ndio waathirika
wakuu wa matatizo yaliyopo kwenye vyuo hivi, Tume imeamua kufuta kibali kilichoanzisha hivi vyuo vikuu vishiriki
viwili yaani: St. Joseph University
College of Agricultural Science and Technology (SJUCAST) na St. Joseph University College of Information
Technology (SJUCIT); na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa
wanasoma katika vyuo hivyo kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT.
Uhamisho huo
pia unahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma digrii za Bachelor of Technology in Agricultural
Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.] na Bachelor of Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.]
ambao hivi sasa wanasoma katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam.
5.
Kufuatia uamuzi huu, wanafunzi wote wanaosoma katika
Vyuo Vikuu vishiriki vya SJUCAST na SJUCIT wanaarifiwa kuwa watahamishiwa
kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na
masomo wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu na masharti yafuatayo:
i) Wanafunzi wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja
baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa
mujibu wa taratibu zilizowekwa.
ii)Wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo
watavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula (semester) wa pili. Tarehe
halisi ya kuanza kwa muhula wa pili kwa kila chuo watakachopangiwa itatangazwa
na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
iii)Wanafunzi
wote wanaosoma digrii ya sayansi za kilimo na uhandisi (programmes related to agricultural sciences and engineering)
watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
iv)Wanafunzi wanaosoma digrii ya ualimu wa sayansi
watahamishiwa katika mojawapo ya vyuo vikuu vifutavyo: Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo
(SUA); Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM); na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
v)Wanafunzi
wote wanaosoma digrii na diploma ya sayansi ya kompyuta watahamishiwa katika
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). vi) Wanafunzi wote wanaosoma digrii ya
ualimu na sayansi ya kompyuta watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki
cha Ruaha (RUCU).
vii)Orodha
ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa itatangazwa
na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.
viii)Wanafunzi
wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa
kwanza, au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa kufanya mitihani hiyo
katika vyuo vikuu watavyohamishiwa kwa utaratibu maalum utakaondaliwa na chuo
husika.
ix)Kila
mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo ya
kitaaluma kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na matokeo ya
mitihani aliyokwishafanya.
x)Wanafunzi wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo wakapokuwa
wamehamishiwa.
6.Kampasi nyingine za Chuo Kikuu cha SJUIT zinaendelea na
masomo kama kawaida.
7.Kwa taarifa hii, vyuo vikuu vyote nchini vinakumbushwa
kufuata sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora
vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa
chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora
kwa kisingizio cha aina yoyote.
Imetolewa na
PROF. YUNUS D. MGAYA
Katibu
Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu
Tanzania
19
Februari 2016
0 comments: